KWA wiki moja hakuna mtu hata mmoja ambaye ameshanipigia simu, nalazimika kuweka dola ili nianze kuwasumbua na kuwakumbusha kuwa bado niko hewani!’
Hiyo ilikuwa kauli ya kijana mmoja tuliyekuwa naye kwenye ukumbi wa michezo, tukifuatilia mechi za Ligi ya Ulaya ambazo kwa siku za karibuni zimewafanya Watanzania kuwa vichaa, kutokana na msisimko wake na kusahau ushabiki ulioshamiri wa Simba na Yanga na ligi yetu ya ubabaishaji kwa ujumla. Kimsingi mshabiki huyo alikuwa akizungumza na rafiki yake, lakini nilisikia hoja yake na jinsi hoja iliyo ilivyozidi kuzua ubishi baina yao, ndipo niliposikia na kuanza kutafakari hatima ya simu zetu na uchumi wetu na kulazimika kuandaa makala hii. Tunalazimika kutafakari hali hiyo kwa sababu inapofikia mtu mwenye simu kukosa mtu wa kumpigia kwa wiki nzima na kulazimika kuingia mfukoni na kutoa fedha kwa lengo la kuwapigia simu jamaa na marafiki zake kuwakumbusha kuwasiliana naye, lazima kuna kasoro ndani ya vichwa vyetu au simu hizi zimetufanya vichaa na wendawazimu. Haja ya mtu kumiliki simu ni ya umuhimu wa pekee na kila anayefikiria kununua simu, lazima atakuwa na sababu za kutosha za kutumia teknolojia hiyo ya mawasiliano ambayo, licha ya kununuliwa kwa kitita kikubwa, pia kinatulazimisha kutumia kiasi kikubwa cha fedha kila siku ya kukiwezesha kuwa hai. Kumiliki simu ya mkononi ni gharama kama ilivyo kwa gharama nyingine inayohitaji bajeti maalumu katika kaya zetu, lakini sidhani kama kila anayemiliki chombo hicho muhimu cha mawasiliano ana bejeti kwa ajili ya kukiwezesha kuwa hewani kila mara na kuwasiliana atakavyo, vinginevyo basi maumivu ya matumizi ya kila siku ya simu yanajulikana kwa kila mmoja wetu kivyake na hakuna anayeweza kumuondoa mwenziwe katika hili. Miaka kadhaa iliyopita, umiliki wa simu ulikuwa ‘mtindo’ au fasheni kama wasemavyo vijana, lakini kwa sasa kila mtu anayeheshimu hadhi yake katika jamii, lazima awe na simu ya mkononi bila ya kujali kama inatumika au haitumiki kama ya rafiki yangu niliyotoa mfano wake hapo juu. Wanafunzi wa shule za msingi, sekondari wanatamani kumiliki simu, lakini baadhi yao wanabanwa na kanuni za shule. Mama wa nyumbani anataka awe na simu, mpiga debe ana haja ya kuwa na simu, machangudoa, wasusi kwenye saloni, utingo, maofisa na kila mtu wa kila kada anatamani kuwa na simu!‘Ukose simu we nani dada aka!’ Alisikika akisema dada mmoja anayefanya kazi za nyumbani kwa kigogo mmoja na kuongeza kuwa hata kama huna wa kuwasiliana naye lakini lazima kiganja chako kiwe na simu, tena ya kileo! Bila ya kujua jinsi kifaa hicho kinavyoathiri maisha yetu kiuchumi, Watanzania wengi tumeingilia fasheni hiyo bila ya kuwa na sababu za msingi na kujikuta tukiteketeza mamilioni ya fedha ambazo tungezitumia kuwaelimisha watoto wetu na wale walio katika mazingira magumu na kuandaa jamii bora baadaye na kuiga maisha ya kifahari ambayo hatujayafikia. Kwa ushawishi wa wamiliki wa mashirika ya mawasiliano yaliyopo nchini, Watanzania tumejikuta tukiingia mkenge kwenye mtego huo unaotuathiri kiuchumi na kuendelea kujivunia hali hiyo bila ya wasiwasi wowote na kwa kutembea kifua mbele huku wengine wakidiriki kutembea na simu mbili au tatu mkononi kwa wakati mmoja.Hii ni fahari.
Ni fahari yenye madhara makubwa kwa taifa na kilio cha serikali kuyataka mashirika yanayotoa huduma za mawasiliano nchini kupunguza gharama za huduma hiyo ili kuwapunguzia walaji wao ughali wa maisha, kimekosa mashabiki na hivyo kuwazidishia ukaidi wamiliki wa makampuni hayo na kushindwa kuona madahara ya bei zao kwa uchumi wa wananchi.
Uwezekano wa gharama za mawasiliano ya simu na zile za Internet kupungua na kutoa ahueni kwa watumiaji wanaozidi kuongezeka kila siku na kukimbilia teknolojia hiyo mpya ya habari na mawasiliano, ni mdogo na kuna kila dalili kwamba uchumi wa Watanzania utazidi kuporomoka licha ya kuwepo kwa mikakati mingi ya kuuinua. Utafiti unaonyesha kuwa hakuna dalili za makampuni yanayotoa huduma hizo kupunguza gharama zake licha ya kuwapumbaza wateja kwa kuwapatia muda wa bure wa hewani na fursa ya kuwasiliana kwa mitandao inayofanana kwa gharama ya sh 1/- kwa sekunde, nyakati fulani na hata kuwa na bahati nasibu za zawadi kubwa hata za magari. Wakati gharama za kutumia mtandao wa internet Dar es Salaam imeendelea kuwa sh 500 kwa saa moja, gharama mjini Morogoro ni sh 800 wakati Mwanza na viunga vyake ni sh 1,500. Hakuna dalili za gharama hizi kupungua bali kuna uwezekano mkubwa wa gharama hizi kupaa kulingana na wamiliki wa biashara hizi wanavyolalamika kila siku juu ya gharama za uendeshaji wa biashara zao. Gharama za kupiga simu kwa dakika moja ni kati ya sh 360 kwa dakika kwa wanaomiliki simu za mkononi na sh 500 kwa wanaotumia simu za vibandani. Viwango hivi ni vikubwa sana ikilinganishwa na vipato vya Watanzania ambao takriban asilimia 90 yao hawana uhakika wa kupata milo miwili kwa siku, watu ambao wastani wa vipato vya wengi wao ni chini ya dola moja ya Marekani. Mazingira ya kuonekana watu wa kisasa na wa karne ya leo na wanaokwenda na wakati yametufunga kwenye gereza la kiuchumi, tunatumia kiasi kikubwa cha fedha kuwasiliana hata kama maongezi yenyewe hayana manufaa au maana yoyote. Tunapoambiwa kuwa njia hii ya mawasiliano inaboresha maisha, ni kwa kiwango gani tumetafakari na kujiridhisha kuwa matumizi ya njia hii ya mawasiliano inaboresha maisha badala ya kuporomosha maisha yetu? Kila siku makampuni yanayotoa huduma hizi yamekuwa yakitumia mabilioni ya fedha za kigeni kusambaza miundombinu ya mawasiliano kufika kila eneo, yanatumia fedha nyingi kuwekeza na kama tunavyojua kila mfanya biashara kila siku anajali kupata faida kutokana na uwekezaji wake. Mabilioni hayo yanahitajika kurejeshwa kwa kila mbinu na mapema mno pamoja na faida kwa wawekezaji na faida hii lazima itokane na kuchangiwa na wanafamilia au wateja milioni nane waliopo kwa mujibu wa takwimu zilizopo.Wawekezaji hawa kila siku wamekuwa wakitengeneza faida kubwa kutokana na biashara huduma za habari na mawasiliano nchini, nani anajua wanapata faida kiasi gani? Hiyo ni siri yao bali sisi tunaona wanatoa muda wa maongezi wa bure, wanatoa vizawadi kwa shule, simu, magari na vitu vingine vinavyotushawishi kuendelea kuchangia mifuko yao. Kwa nini waeleze faida wanazopata? Unapomkamua ng’ombe ni lazima umfanye ng’ombe aamini kuwa anayenyonya maziwa yake ni ndama wake na wala si bwana wake, ufanye kila hali kumuaminisha kuwa haibiwi! Haya ndiyo mazingira tuliyojengewa na wawekezaji hawa na kila siku tunajipanga foleni kununua simu nyingine mpya na kununua muda wa maongezi bila ya kufuata bajeti zetu.Tuna watoto wanaotaka kusoma kwenye shule bora, wanataka kulala sehemu nzuri na kuvaa vizuri; tunawazazi wetu wanaohitaji kutunzwa na kuishi maisha mazuri; tunahitajika kuwa na nyumba nzuri ya kifamilia na kutekeleza mambo mengine muhimu ya kifamilia, lakini tumejiingiza kwenye ulevi huu na sasa unazorotesha uchumi wetu bila ya kujua! Wamiliki wa makampuni haya wamekuwa wakilaumu viwango vya kodi vinavyotozwa na serikali kuwa chanzo cha gharama kubwa kwa huduma hii ambayo hatutarajii kuiacha ingawaje taarifa zinaonyesha kuwa kati ya asilimia 25 na 30 za kodi zinazolipwa na wakazi wa nchi za Afrika mashariki ukilinganisha na wakazi wan chi nyingine barani Afrika ambao hulipa asilimia 17. Kimsingi, biashara ya huduma ya maongezi kwa njia ya simu haina mapatano na ukweli kwa sababu licha ya makampuni haya kubainisha bayana viwango vya kutoa huduma hiyo kwa sekunde au dakika, lakini maamuzi ya kiwango kilichotumiwa na mteja yanabakia kuwa kwa mtoa huduma, hivyo ana uhuru wa kukata kiwango chochote na wewe kama mteja huna pa kupeleka malalamiko yako. Watatangaza kuwa viwango vyetu ni kiasi fulani bila ya kujumuisha kodi ya ongezeko la thamani (VAT), basi ni juu ya mteja kukubali au kukataa na kama utakubali kutumia huduma hiyo, basi malalamiko yako yatakayojitokeza baada ya kutokutendewa haki kwenye makato yatakuwa yako binafsi bila ya kuwa na mtu wa kusikiliza malalamiko yako. Wakati tunapotafakari hali ya umaskini uliolighubika taifa letu na kutuingiza ndani ya utumwa kwenye taifa hili huru ni wakati mwafaka kwetu kuanza kujiwekea mikakati ya kupunguza matumizi yetu kama kweli tunataka kuinua uchumi wetu kifamilia na kitaifa. Fedha tunazotumia kwa ajili ya kupiga simu na mawasiliano ya Internet ni kikwazo kikubwa kwa uchumi wetu kwa sasa! Ni vema tukaangalia tena bajeti zetu na kutumia kulingana na kipato chetu na hivyo kuacha uhayawani wa kubebana na simu tatu mkononi. Ni vema ujue kuwa unapokuwa na simu zote hizo unalenga kufanya nini, kwani huwezi kuwasiliana kwa simu moja na hizo nyingine ukaziuza na fedha inayopatikana ikatumika kuokoa maisha ya yatima wanaokwenda bila ya kula au wanafunzi wanaokaa sakafuni kwa kukosa madawati kwenye wilaya yako. Ingawaje biashara hii inafanyika ndani ya soko huria na huru, na kutokana na utashi na haki za kikatiba za mawasiliano na kupata habari tuliyo nayo, bado serikali yetu inatakiwa kuendelea kuwabana wawekezaji hawa kupunguza gharama za kutoa huduma hizi za mawasiliano badala ya kuendelea kuturubuni na vizawadi vidogovidogo huku wakitutafuna na kutubakiza mifupa. Kama leo baadhi ya makampuni yanadiriki kutoa huduma ya mawasiliano kwa sh.1/- kwa sekunde na bado wanatengeneza faida, hebu fikiria kiasi walichokusanya wakati walipokuwa wakitoza sh.6 kwa sekunde. Naamini kuwa teknolojia hii licha ya kuturahisishia mawasiliano na upatikanaji wa habari lakini kwa kiwango kikubwa imetudumaza kiuchumi. Tunataka sana kuwasiliana lakini huduma hii itolewe kwa gharama nafuu, ili lengo kuu la kuboresha maisha liwezekane kinyume na hivyo basi tutaamini kuwa utandawazi nao ni aina nyingine ya unyonyaji na hivyo kuanzisha vita dhidi ya utandawazi.
Sunday, June 28, 2009
Matumizi ya simu za mkononi hayaendani na vipato vya wengi
KILA mtu katika jamii anahitaji kuwa na maendeleo, ikiwa ni moja ya hali za kuiridhisha nafsi yake.
Tunapozungumzia maendeleo tunalenga mabadiliko katika mwenendo mzima wa maisha ya mwanadamu, baada ya kujibidisha kufanya jambo la kuleta badiliko hilo jema.
Inasikitisha kusikia kwamba nchi yetu ni moja ya nchi maskini duniani na kuangukia kwenye kundi la nchi zinazoendelea.
Kwa maana hiyo basi, ni lazima kuwe na vigezo vya mtu kuonekana ameendelea kutoka hatua fulani ya maisha hadi nyingine.
Kwa mfano, kama jana kwenye mtihani wa hisabati ulipata alama 30 na katika mtihani wa leo umepata 40, basi hapo tunasema ameanza kuwa na maendeleo.
Vile vile mfugaji ambaye mwaka jana alikuwa na ng’ombe watano lakini mwaka huu ana ng’ombe 10, naye pia ana maendeleo mazuri.
Kabla ya Serikali ya Awamu ya Pili, Tanzania ilionekana maskini sana, lakini mara baada ya kuruhusa kuingiza bidhaa ambazo awali zilionekana si za muhimu kwa ustawi wa Mtanzania tulishangaa kuona nchi imebadilika ghafla kimuonekano.
Mwaka 1987 tukaanza kusikia na kuona luninga, majokofu, magari ya kifahari, vipodozi vya kila aina na nguo za kila namna na hapo kila mwenye uwezo alinunua kile alichokifurahia.
Baada ya muda fulani zikaingia simu za mkononi, maarufu kama mobiteli.
Kutokana na kuwa ghali kila aliyekuwa nayo alihesabika ameendelea au mwenye uwezo wa kifedha.
Kisaikolojia waliokuwa na simu walionekana kama watu wa kipekee na ndiyo maana kila aliyepata fedha zake alinunua simu kwa gharama ya kujinyima hata kula.
Hata hivyo kadiri teknolojia ya mawasiliano ya kisasa ilivyopanuka na kuenea ilionekana kuwa Watanzania walikuwa mstari wa mbele kuichangamkia. Kwa maana ni watu wanaopenda maendeleo.
Walio wengi maendeleo yakawa ni kuwa na simu na wala si jambo jinginelo katika maisha ya kila siku.
Katika maisha ya kawaida ya mfanyakazi wa kima cha kawaida inaaminiwa kuwa kipato chake ni wastani wa dola moja ya Marekani.
Lakini uhalisia wa matumizi ya kumuwezesha kuishi akiwa amejipatia japo kipoza njaa, gharama yake ni takriban dola tatu kwa siku.
Mchanganuo katika familia moja ya kawaida, yaani baba, mama na watoto wanne kwa matumizi ya mwezi yanafanana kama ifuatavyo:
Chakula ni wastani wa sh 150,000; kodi ya nyumba ni sh 20,000; kuchangia umeme sh 20,000; maji sh 30,000; na nauli ya baba kwenda kazini na kurudi ni sh 30,000 na matumizi mengine sh 10,000; jumla ya vyote ni sh 260,000 kwa mwezi.
Sasa tuitazame hii familia ambayo baba kipato chake hakizidi sh 120,000 wa mwezi tena akiwa amebahatika kuwa na mwajiri mwenye utu.
Sasa kama bajeti nyingi zinafanana, hivi watu wanaishije majumbani mwao hata tunawaona wakiwa barabarani kila siku?
Hapo wengine tunakuwa na alama za kuuliza na kutuaminisha kwamba bila shaka baba yule ana namna nyingine za kuongezea kipato.
Iwe kupitia kwa shughuli anazofanya mkewe za kuuza mandazi au yeye hujiongezea kipato kwa kumdanganya mwajiri wake na pengine kumwibia kabisa.
Lakini tukiwa na bajeti hiyo kichwani, hebu tuone pia kuwa kila Mtanzania anajibidisha kuwa na simu ya kiganjani ambayo inaongeza mzigo wa matumizi yasiyoepukika ili mtu aone maana ya kuwa na kifaa hicho.
Kwa kadiri makampuni ya biashara ya simu yanavyosukumwa na upepo wa ushindani wa kibiashara, kidogo kumekuwa na unafuu wa gharama za kumiliki na kutumia simu binafsi.
Hata hivyo matumizi ya simu yanatofautiana kati ya mtu na mtu maana wengi hasa wafanya biashara huzitumia simu kwa mawasiliano ya utafutaji wa pesa, si kutumia pesa bila kuingiza pesa.
Lakini bado wapo wanaowasiliana kwa maana ya kujuliana hali na kupeana taarifa fulani za kimaisha.
Ingawa bajeti zetu kwa kweli ni ngumu lakini watu bado tumeng’ang’ania chombo hiki.
Kama nilivyoeleza kuwa mara nyingi matumizi ya simu nayo yanaweza yakaongozwa na uwezo wa mtu kifedha, kwani wapo wanaotumia wastani wa sh za Tanzania zisizopungua 30,000 au zaidi kwa siku moja.
Na kwa walalahoi walio wengi hujibana akijitahidi ili atumie wastani wa sh 1,000 kwa siku, hata, hivyo wakati mwingine hudai hana mtu wa kumpigia.
Gharama hii kwa mwezi yaweza ikawa sh 30,000 na tukiongeza katika bajeti yetu pale juu tunapata jumla ya sh 300,000.
Je, familia hii haioni kuwa ina kuwa na maisha magumu kila wakati kwa kushindwa kuishi kulingana na kipato?
Bajeti hii ambayo hailingani na vyanzo vya mapato ndivyo vinavyomsaidia ibilisi kumwingia mtu ashiriki kufanya maovu ili awe na kipato cha kukidhi hitaji la bajeti.
Kumbuka bajeti yetu haina gharama kwa ajili ya watoto kwenda shule kila siku sasa wewe msomaji utatafakari hilo mwenyewe.
Lakini pengine niwashawishi wenzangu kuwa ni heri mtu ujiweke katika maisha yanayolingana na unachopata ili usiije ukashawishika kuingia majaribuni na kuwakosea wanadamu na hata Muumba wako.
Ni kweli, kuwa na jokofu, gari, luninga na simu, vyote ni vya maana na muhimu kwa maisha yetu ya kila siku lakini ni vizuri zaidi kujipima ubavu wa kuwa na vitu hivyo.
Kuna rafiki yangu mmoja alinineleza atamuomba mjomba aliye nje ya nchi amletee gari ili naye aweze kuzalisha pesa.
Lakini nilimwambia rafiki yangu kuwa wazo lake ni jema lakini endapo atabahatika kuletewa gari kwa hali aliyonayo hatamudu kulifanya litembee barabarani.
Baada ya rafiki yangu kufikiria gharama ya mafuta pekee lakini akasahau kuwa kuna zaidi ya mafuta ili gari liwe barabarani kila siku.
Si nia yangu katika makala hii kuwakatisha tamaa Watanzania wanaodhani kuwa kumudu kununua simu ndiyo yote katika yote bila kufikiria gharama za muda wa maongezi za kila wakati ili ilete maana ya mtu kuwa na simu.
Ili maendeleo haya yasiwe mzigo wa kupasua vichwa vyetu, ningedhani ni vema tusijiingize kuiga maendeleo ya juu kabla ya kutosheleza bajeti zetu za kila siku, hususan hitaji la ugali na shule kwa watoto.
Nisingependa kulaumu walio na bahati mbaya ya kuwa na simu kwa kufuata mkumbo bali naamini kila mtu afungapo safari huwa tayari amekuwa ameagana na kisigino chake kwa ajili ya safari hiyo.
Binafsi nimeliona tatizo la kwamba simu zetu zinafanya maisha kuwa magumu siku kwa siku, maana watu hutumia gharama hata kupunguza bajeti ya mlo wa nyumbani.
‘Kupanga ni kuchagua,’ lakini hekima inatakiwa katika maamuzi tunayofanya.
Tuwe na simu na tuzitumie kadiri kipato kinavyoturuhusu.

Subscribe to:
Posts (Atom)