Header

Tangazo la ajira Wizara ya Afya, Tanzania

Serikali inaendelea kufanya maboresho ya Sekta ya Afya kupitia Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) ikiwa ni pamoja na kuongeza vituo vya kutolea huduma, kuongeza idadi ya watumishi pamoja na kuboresha maslahi ya watumishi. Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ametoa Kibali cha Ajira kwa Wataalam wa Kada za Afya 9,391 kwa mwaka wa fedha 2011/2012 ili kutekeleza azima hii, Katibu Mkuu, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, anapenda kuwatangazia wale wote wenye taaluma zifuatazo:-

Madaktari, Madaktari Bingwa, Wafamasia, Maafisa Wauguzi, Wauguzi, Maafisa Afya ya Mazingira, Wateknolojia wa Maabara/Mionzi/Dawa, Maafisa Tabibu na Matabibu Wasaidizi na Kada nyinginezo za Afya kwamba, Wizara ipo tayari kuwapangia kazi.

Wahitimu waliofuzu Mafunzo ya Afya, katika mwezi Julai, 2011 watapangiwa kazi moja kwa moja na hawatalazimika kutuma maombi.Majina ya waliopangiwa vituo vya kazi yatatangazwa kwenye Magazeti na Tovuti ya Wizara www.moh.go.tz. Pia Wahusika watatumiwa barua za kupangiwa kazi katika anuani zao za posta, na kwa waajiri wao watakakopangiwa.

Aidha, Waombaji wengine wanatakiwa kutuma maombi yao kwa Katibu Mkuu kwa kutumia Anuani iliyotajwa hapa chini. Muombaji anatakiwa kuwa na sifa zifuatazo:-

  1. Awe ni raia wa Tanzania.
  2. Awe na umri usiozidi miaka 45.

Waombaji wanashauriwa kupendekeza Halmashauri tatu ambazo wangependa kupangiwa kazi. Hata hivyo Wizara itatoa kipaumbele zaidi kwa Halmashauri zilizopo nje ya Dar es Salaam, na upangiwaji wa vituo utategemea uwepo wa nafasi wazi katika Halmashauri hizo.

Maombi yote yaambatanishwe na:-

  1. Nakala ya Cheti cha Taaluma
  2. Nakala ya Cheti cha Kidato cha nne/sita
  3. Maelezo binafsi (CV) ikijumuisha anuani kamili, umri na namba ya simu ya kiganjani.
  4. Picha (Passport size mbili) za hivi karibuni
  5. Nakala ya Cheti cha usajili kutoka baraza la taaluma husika.

Vyeti vyote vya Taaluma na Kidato cha nne/sita vithibitishwe na Hakimu au Wakili.

Barua zote zitumwe kwa:-

Katibu Mkuu,
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,
S.L.P. 9083,
DAR ES SALAAM.